Pale wakati wa kilele cha vita vya Har-Magedoni, ambayo ni siku ya mwisho wa dhiki kuu, Yesu Kristo ataingia kwenye uwanja wa vita akiwa kwenye farasi mweupe. Yeye atakuwa ameandamana na jeshi lake la mbinguni. Twaambiwa hivi katika Ufunuo 19:11-16:
"Kisha nikaziona mbingu zimefunuka, na tazama farasi mweupe, na yeye aliyempanda aitwaye mwaminifu na wa-kweli, naye kwa haki ahukumu na kufanya vita. Na macho yake yalikuwa kama mwali wa moto, na juu ya vichwa vyake vilemba vingi; naye ana jina lililoandikwa, asilolijua mtu ila yeye mwenyewe. Naye amevikwa vazi lililochovywa katika damu, na jina lake aitwa, Neno la Mungu. Na majeshi yaliyo mbinguni wakamfuata , wamepanda farasi weupe na kuvikwa kitani nzuri, nyeupe, safi. Na upanga mkali hutoka kinywani mwake ili awapige mataifa kwa huo. Naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, naye anakanyaga shinikizo la mvinyo ya ghadhabu ya hasira ya Mungu mwenyezi. Naye ana jina limeandikwa katika vazi lake na paja lake, MFALME WA WAFALME, NA BWANA WA MABWANA."
Baada ya adui mpinga Kristo kushindwa katika vita, na wale manabii wa uongo na wafuasi wake kuhukumiwa (Ufu.19:20-21), shetani atafungwa na kuwekwa kizuizini:
"Kisha nikaona malaika akishuka kutoka mbinguni, mwenye ufunguo wa kuzimu, na mnyororo mkubwa mkononi mwake. Akamshika yule joka, yule nyoka wa zamani, ambaye ni ibilisi na shetani, akamfunga miaka elfu; akamtupa katika kuzimu, akamfunga, akatia muhuri juu yake, asipate kuwandanganya mataifa tena, hata ile miaka elfu itimie; na baada ya hayo yapasa afunguliwe muda mchache" (Ufu. 20:1-3).
Pale msalabani, ushindi mkuu ulipatikana katika vita na muovu shetani. Inatubaidi tukubali tukio hili kwamba tayari muovu ameshindwa, kwa imani na kuishi maisha ya ushindi. Lakini hii haimanishi kwamba muovu shetani hayuko tena. La hasha! hata mtume Petro anatuonya kwamba muovu, kama simba yuko anatembea huku na kule akitafuta ni nani atamuangamiza. Twasoma hivi:
"Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshataki wenu ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka zunguka, akitafuta mtu ammeze" (1 Pet. 5:8).
Onyo hili ni kwao waKristo ili wajiandae na kuwa tayari kukumbana na muovu huyu wakati wowote anapojitokeza. Tunaweza kupata ushindi kila wakati tunapokumbana na muovu pale tu tunapoishi kwa karibu kabisa na mwokozi wetu Yesu Kristo, na kupambana kujiepusha na njama zake. "Basi mtiini Mungu. Mpingeni shetani, naye atawakambia" (Yak. 4: 7).
Imani ile ambayo Mkristo huwa nayo, imani inayomfanya asitishwe na muovu, sio imani inayotajwa ya miaka elfu moja. Imani Mkristo aliyo nayo wakati huu ni kwa ajili Mungu, kupitia Kristo anaweza kumshindia. Imani ile ya miaka elfu moja ni imani ambayo imetokana na sababu kwamba muovu tayari ameshindwa, akawekwa kizuizini na hata hawezi tena kutembea na kuhangaisha wateule wa Mungu. Hivi sasa vita vilivyoko ni vya imani (spiritual battle).
Twasoma hivi katika kitabu cha Waefeso: "Vaeni silaha zote za Mungu mpate kuweza kuzipinga hila zote za shetani" (Efe. 6:11-12).
Kwa kweli, hata Kristo aligusia jambo hili akasema hivi katika Mathayo 10:34: "Msidhani yakuwa nimekuja kuleta amani duniani; la! sikuja kuleta amani, bali upanga."
"Kwa hivyo, imani tuliyonayo ni ya kutoka kwake Mungu na inapatikana mioyoni mwetu sisi walio na imani. Imani hii ndio inayotusaidia kupigana na uovu ulioko duniani."
Twasoma hivi katika 1 Yoh. 5:19: "Twajua ya kuwa sisi tu wa Mungu; na dunia yote hukaa katika yule muovu."
Katika wakati ule wa dhiki kuu, twasoma katika Ufu. 12:12 kwamba muovu atazidisha jitihada zake, na kushurutisha mataifa mengi duniani yachukue silaha na kuelekea mashariki ya kati katika jaribio la kuangamiza taifa la Israeli. Yohana ametaja jambo hili kwa urefu:
"Nikaona roho tatu za uchafu zilizofanana na vyura, zikitoka katika kinywa cha yule joka, na katika kinywa cha yule mnyama, na katika kinywa cha yule nabii wa uwongo Hizo ndizo roho za mashetani, zifanyazo ishara, zitokazo na kuwaendea wafalme wa ulimwengu wote kuwakusanya kwa vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi" (Ufu. 16:13-14).
Na pale Kristo atakaporudi, ndipo shetani atashindwa kabisa. Yule mnyama na nabii wa uongo watafungwa katika ziwa la moto. Naye yule mnyama (dragon) atatupwa katika shimo refu kabisa. Lenye giza akiwa amefungwa na minyororo. Atakaa huko kwa muda wa miaka elfu moja.
Mtume Mathayo anaeleza kwa undani jinsi vile hukumu itatolewa pale Kristo atakaporudi na kukaa katika kiti cha enzi.
"Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake; na mataifa yote watakusanyika mbele zake; naye atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi" (Mt. 25:31-32).
Hukumu ya Kristo itakuja pamoja na mpangilio mpya wa kimataifa. Mataifa fulani yatapanda, mengine kushushwa. Na hii itaambatana na vile mataifa haya yamehusiana hapo awali na taifa la Israeli.
Baada ya Kristo kurudi tena duniani, sherehe ya arusi ya mwana kondoo huyu itaandaliwa duniani. Kuhusu jambo hili, Mtume Yohana anasema hivi:
"Na tufurahi, tukashangalie, tukampe utukufu wake; kwa kuwa arusi ya Mwana-Kondoo imekuja, na mkewe amejiweka tayari. Naye amepewa kuvikwa kitani nzuri, ing'arayo, safi; kwa maana kitani nzuri hiyo ni matendo ya haki ya watakatifu" (Ufu. 19:7-9).
Wakati atakaporudi bila kujionyesha kabla ya dhiki kuu, Kristo ataungana na mwenzake. Naye huyu atakutana na Yesu angani. Baada ya miaka saba ndipo Kristo na mwenzake katika arusi atajitokeza na kuonekana. Sherehe ya arusi itawaleta pamoja wageni wengi maalum. Kati ya hawa ni waisraeli ambao watakuwa wamemkubali Kristo kuwa mwokozi pale siku za mwisho za dhiki kuu.
Kwa vile Kristo atakuwa amerudi duniani na mwenzake wa arusi kutoka angani na kumjulisha kwa wageni walioko duniani, yale ambayo yametajwa katika wakolosai yatatimia.
"Kristo atakapofunuliwa, aliye uhai wetu, ndipo na ninyi mtafunuliwa pamoja naye katika utukufu" (Kol. 3:4).
Na kwa njia hii, kanisa litakuwa naye pamoja katika kusheherekea ushindi mkuu, na kuvunjilia mbali nguvu za muovu shetani mkuu na kuanzisha ufalme wa wema duniani.
Katika enzi ya miaka elfu moja (millennial), kanisa la Kristo litatawala naye hapa duniani. Wazee ambao ni ishara ya kanisa takatifu wanaozingira kiti cha enzi katika Ufunuo 5 watazamia kwa hamu na kungoja wakati ule Kristo ili wachaguliwe kuwa wafalme katika enzi hii.
"Kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme wa makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi" (Ufu. 5:9-10).
Katika Luka 19:11-28, twasoma pia kuhusu utawala huu mpya wa Kristo na wateule wake. Mkuu yule aliyesafiri nchi za mbali na baadaye kurudi bila shaka ni Yesu. Ni yeye ambaye wakati wake kuja mara ya kwanza hakutambuliwa kuwa mfalme. Akiwa mtumishi mnyenyekevu na mwana kondoo wa Mungu, yeye aliyatoa maisha yake kwa ajili ya wenye dhambi. Na alipokufa na baadaye kufufuka alienda safari ya mbali kuwa naye Mungu, ambapo alipokea sifa zote na heshima za mbinguni (Wafilipi 2:9).
Atakaporudi duniani kama mfalme, yeye naye, pia atawachukua wafanyi kazi wake kuwa kuwa kama wafalme. Mmoja atapewa mamlaka juu ya miji kumi, mwenzake naye juu ya miji tano, naye yule ambaye atakuwa hajatimiza wajibu wake na kuja mbele ya Kristo mkono mtupu hatapewa mamlaka.
Ufalme huu si wa mbinguni tu; bali ufalme huu utakuwa pia hapa duniani. Kiti cha enzi kitakuwa kile cha Daudi katika mji wa Yerusalemu. Na haya twayapata kutoka kwa yale malaika aliyanena mbele yake Mariamu kwamba: "Tazama utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha daudi, baba yake" (Lk. 1:31-32).
Ufalme wake Daudi hauko mbinguni ila ni katika nchi ya Israeli, mjini Yerusalemu. Ufalme wa Kristo nao utaenea hadi kila pembe ya dunia. Ingawa hali itakuwa shwari yenye usalama, kutakuwa na haja kuwa na sheria kali kudumisha hali hiyo. Na hii ni kwa sababu wako wengi ambao watakuwa bado hawajaokoka ambao a watakuwa wameepuka dhiki kuu. Juu mbinguni, hakutakuwa na utaratibu wa watu kufuata sheria kwa kulazimishwa.
Kristo atakaporudi tena, yeye atakuwa mwenye mamlaka (Isa. 9:6). Kuja kwake kutatangazwa kutoka mbinguni (Ufu.11:15). Katika Ufunuo 12:15, twaambiwa kwamba yeye atatawala na uwezo mkuu, na katika Ufunuo 2:25-27, twasoma hivi:
"Ila mlicho nacho kishikeni sana, hata nitakapokuja. Na yeye ashindaye, na kuyatunza matendo yangu hata mwisho, nitampa mamlaka juu ya mataifa, naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, kama vyombo vya mfinyanzi vipondwavyo, kama mimi nami nilivyopokea kwa baba yangu."
Katika kitabu cha Matendo ya Mitume tumeambiwa wazi kwamba Kristo atarejesha ufalme wa Daudi: "Baada ya mambo haya, nitarejea, Nami nitaijenga tena nyumba ya Daudi iliyoanguka. Nitajenga tena maanguko yake, Nami nitaisimamisha; ili wanadamu waliosalia wamtafute Bwana, Na mataifa yote ambao jina langu limetajwa kwao" (Mdo. 15:16-17).
Wakati ule wa ufalme, kiti cha ufalme kilichoko mjini Yerusalemu patakuwa ndipo mahali pa ujuzi, mamlaka na wema. Nabii Isaya akigusia jambo hili anasema:
"Na itakuwa katika siku za mwisho, mlima wa nyumba ya BWANA utawekwa imara juu ya milima; nao utainuliwa juu ya vilima; mataifa yote yatauendea makundi makundi Na mataifa mengi watakwenda na kusema, Njooni, twende juu mlimani kwa BWANA, nyumbani kwa Mungu wa Yakobo, naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito yake maana katika sayuni itatoka sheria, na neno la Bwana katika Yerusalemu. Naye atafanya hukumu katika mataifa mengi, atawakemea watu wa kabila nyingi; nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe" (Isa. 2:2-4).
Hali kama hii ambapo hakuna matata wala vita wala utengenezaji wa zana za kivita haujawahi kuwako duniani. Hali hii itatokea tu pale malkia wa amani atakaporudi duniani. Na pale atakaporudi, kazi yake ya kwanza itakuwa kumshika mkuu wa enzi hii ambaye ni Mungu bandia na kumfunga mateka. "Mkuu huyu wa dunia na mashetani wa aina aina ndio watawala wa dunia" (Efe. 6:12).
Na kwa vile muovu atakuwa amekamatwa na kubanwa, hataweza kuuhadaa ulimwengu jinsi vile anavyofanya hivi sasa (Ufu. 20:2-3). Matokeo ni kwamba hakutakuwa na vita na ugomvi tena duniani. Uasi wa aina yeyote utaisha and dunia yote itakuwa na imani ya kiKristo.
"Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua BWANA, kama vile maji yanavyoifunika bahari" (Isa. 11:9).
Yerusalemu itachukuliwa kuwa makao makuu ya dunia. Tofauti za kisiasa hazitakuwako.
"Wakati ule watauita Yerusalemu Yerusalemu kiti cha enzi cha BWANA; na mataifa yote watakusanyika huko Yerusalemu, kwa ajili ya jina la BWANA; wala hawatakwenda tena kwa ukaidi wa moyo wao mbaya" (Yer. 3:17).
Jambo baya litakuwa tuu kwamba mataifa fulani hayatakuwa yenye kuheshimu na kufuata mafunzo ya kikristo na moyo wote. Na kwa vile hawa watakuwa walegevvu kufuata maadili ya Kikristo, basi itabidi yatawaliwe kwa nguvu na kushurutishwa kutenda yaliyo mema mbele ya Mungu. Hata huenda yakaadhibiwa kwa ajili ya kutokuwa na uaminifu na hamu ya kutenda yale wanayotarajiwa kutenda.
"Hata itakuwa, ya kwamba kila mtu aliyesalia wa mataifa yote, waliokuja kupigana na Yerusalemu, atakwea mwaka baada ya mwaka ili kumwabudu mfalme, BWANA wa majeshi, na kuishika sikukuu ya vibanda. Tena itakuwa ya kwamba mtu awaye yeyote wa jamaa zote zilizomo duniani, asiyekwea kwenda Yerusalemu ili kumwabudu Mfalme, BWANA wa majeshi, mvua haitanyesha kwao" (Zek. 14:16-17).
Kwa hivyo, ni wazi hapa kwamba ingawa shetani hatakuwako kuwapotosha wanadamu, wanadamu wenyewe bado wako na lile umbo la asili la kutaka kutenda kinyume cha matarajio yake Mungu, kwa hivyo bado kutakuwako hamu ya kuwakosoa wanaotenda uovu ili uhusiano unaofaa na Mungu uendelee kudumu. Wanadamu watahitaji kukuwa kiroho kwa vile miili yetu wanadamu ni ile ya kupenda uovu.
Katika Zekaria 14:16-17, wateule watakuwa wamepona maafa ya vita vya Har-Magedoni na ingawa watakuwa hawajakubali alama ya yule mpinga Kristo, bado watakuwa si wa Kristo hadi pale watakapomkubali kiroho na kwa ukweli kwamba ni yeye mwokozi. Na hapa watapokea wokovu. Kazi ya kueneza injili kati yao itakuwa ni ya wateule wa taifa la Israeli, ambao ingawa wao ni wanadamu sawa na wenzao, tayari watakuwa wamepokea wokovu.
Upo ukweli katika usemi kwamba twatarajia ufufuo mara mbili. Wale watakaofufuka jinsi vile imetajwa katika Luka 14:14 na 1 Thes. 4:16 pamoja na wale watakaopoteza maisha yao kwa ajili aya imani wakati wa dhiki watatawala na Kristo.
"Hao wafu waliosalia hawakuwa hai, hata itimie ile miaka elfu. Huo ndio ufufuo wa kwanza. Heri, na matakatifu, ni yeye aliye na sehemu katika ufufuo wa kwanza; juu ya hao mauti haina nguvu; bali watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, nao watatawala pamoja naye hiyo miaka elfu" (soma Ufu. 20:5-6).
Wakati Kristo atakaporudi, shetani hatatupwa kwenye ziwa la moto kama vile atakavyotupwa mpinga Kristo na nabii wa uongo. Sababu yake yeye kufungwa na kamba kwanza ni kwamba baada ya muda ule maalum wa miaka elfu moja (millennium), yeye atawaachiliwa ili arudi na kusaidia kuwafichua wale ambao bado hawajaokoka. Ni kupitia njia hii waliokoka na wasiokoka wataweza kutambuliwa.
"Na hiyo miaka elfu itakapokwisha, shetani atafunguliwa, atoke kifungoni mwake; naye atatoka kuwadanganya mataifa walio katika pembe nne za nchi, Gogu na Magogu, kuwakusanya kwa vita, ambao hesabu yao ni kama mchanga wa bahari. Wakapanda juu ya upana wa nchi, wakaizingira kambi ya watakatifu, na mji huo uliopendwa. Moto ukashuka kutoka mbinguni, ukawala. Na yule ibilisi, mwenye kuwadanganya, akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti, alimo yule mnyama na yule nabii wa uongo. Nao watateswa mchana na usiku hata milele na milele" (Ufu. 20:7-10).
Mwisho wa muda huu ndio mwisho wa sehemu ya sita ya sehemu saba zilizoko katika mipango yake Mungu. Nazo ni:
1. Kuenea kwa wasio na kosa paradiso.
2. Kuenea kwa mwanadamu mwovu ambaye ameelekezwa katika uovu na moyo wake mwenyewe.
3. Kuenea kwa sheria (law) katika taifa la Israeli.
4. Kuenea kwa wema na neema (grace) kwa kujificha wakati wa kuenea kanisa la Kristo.
5. Kuenea kwa ufalme wa mpinga Kristo wakati wa dhiki kuu.
6. Kuenea kwa ufalme wa Kristo duniani kwa muda wa miaka elfu moja (millennium).
7. Wema wa milele.
Kwa muda mrefu, wale ambao hufuata njia ya wema huwa wachache. Hali hii itaendelea kuwa hivyo wakati ule wa miaka elfu moja ya millennium. Ingawa wengi watafurahia maisha katika enzi hii ya kumjua Kristo, wengi hawatanyenyekea na kumtii Kristo na kuzaliwa mara ya pili. Na pale shetani atakapoachiliwa baada ya muda wa miaka elfu moja, wale ambao hawajapata wokovu watamfuata. Naye shetani hapa atawachukua na kuwashiwishi na kuwafanya waungane naye kupigana vita na Kristo pamoja na wateule wa Mungu ambao wameokoka. Ni katika vita hivyo mwovu pamoja na wafuasi wake wataona cha mtema kuni.
Baada ya miaka ile elfu moja, kiti cheupe cha enzi kitaonekana mbinguni. Ufufuo wa pili utatokea, na wale ambao hawajakumkubali Kristo kuwa mwokozi wata hukumiwa kifo jehenamu. Njia ile zitakutana Yerusalemu, na kutoka hapo moja kuelekea mbinguni, na nyingine katika ziwa la moto wa milele. Haya yanapatikana katika Ufunuo 20:15:
"Na iwapo mtu yeyote hakuonekana ameandikwa katika ktabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto."
Baada ya hukumu mbele ya kiti cha enzi cheupe, dunia itachomwa, na mbingu nayo kutoweka kama karatasi. Dunia na anga mpya itajitokeza. Yerusalemu mpya ambayo Kristo amewaagiza wale wampendao na kumuamini itatoka mbinguni na kuja katika dunia hii mpya.
Mji huu una barabara ambazo zimejengwa kwa kutumia dhahabu. Misingi yake imejengwa na mawe maalum ya thamani kubwa. Mji huu umezingirwa na ukuta ulio na milango kumi na mbili. Mawe ya ukuta huu ni ya thamani na yanametameta. Kila mlango una umbo sawa na ule wa lulu (pearl). Lulu hutokea pale mnyama shaza au kombe ya pwani (oyster) anapoumizwa. Wakati shaza huyu anapumizwa kwa njia fulani, basi pale ambpao ameumia hujijenga na kuwa lulu. Uchungu wake huleta kitu cha thamani kubwa. Kristo naye pia kupitia maumivu ya pale msalabani ameweza kuleta makuu kwetu sisi wanadamu. Nii kupitia mlango huu uliotengenezwa kwa mfano wa kiti cha thamani kubwa sana ambacho ni lulu tunaweza kuingia katika Yerusalemu mpya, na hapa kuingia katika ufalme wa mbinguni na kufurahia kuishi katika utukufu wa Mungu.
Tunaonyeshwa wazi ambavyo dunia na mbingu mpya ilivyo katika Ufunuo 22. Baada ya kuonyeshwa haya yote, tunarudi tena katika nyakati za sasa. Baada ya kuyaona hayo yote, na hata yale yatakayowakumba wasiokuwa na imani, msomaji sasa anahitajika kuchukua msimamo maalum. Mungu anamtaka kila mmoja wetu ajiandae kwa ajili ya kurudi kwake Mwokozi wetu. Ni wajibu wetu kuishi maisha ya kumtii Mungu, kuwa wafuasi halisi, na kujiweka mbali sana na uovu ulioko duniani wakati huu. Twasoma hivi katika Ufunuo 22:10-12:
"Akaniambia, Usiyatie muhuri maneno ya unabii wa kitabu hiki, kwa maana wakati huo umekaribia. Mwenye kudhulumu na azidi kudhulumu; na mwenye uchafu na azidi kuwa na uchafu; na mwenye haki na azidi kufanya haki; na mtakatifu na azidi kutakaswa. Tazama, naja upesi, na ujira wangu U pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo."
Naye mtume Paulo ana ujumbe kama huu katika Tito 2:11-14: "Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa; tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na mwokozi wetu; ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote, na kujisafishia watu wawe milki yake mwenyewe, wale walio na juhudi katika matendo mema."
Katika Ufunuo, tunakumbushwa haifai tung'ang'anie umoja jinsi ambavyo waBabeli huamini. Wengi hutafuta umoja kwa njia zote, lakini ukweli ni kwamba katika nyakati hizi ambapo kuna wema na uovu duniani, hatuwezi tukawa na umoja. Kile ambacho lazima tuwe tayari kukumbana nacho ni hali kubwa ya kutoelewana kati ya wale wanaotenda wema na wale watendao uovu. Mkristo anafaa kujiandaa kikamilifu kwa kukumbana na hali hii ya kutoelewana. Lazima mtu aachilie mbali uovu wote ulioko katika jamii, na kujitenga kabisa.
Ni jambo la muhimu kufuata njia ya wema ambayo ni nyembamba na ya taabu nyingi. Usihangaike wala kusumbuka pale wengi ambao wamepotoka na hata wako katika baadhi ya makanisa yetu siku hizi wanapokufanyia dhihaka kwa ajili ya msimamo wako. Kumbuka wakati Kristo alipokuwa hapa duniani, hata yeye alifanyiwa dhihaka. Kristo mwenyewe ametufahamisha wazi kwamba wafuasi wake nao pia lazima watapata shida (Yoh.16:33). Wakristo walio na imani hafifu hawatahukumiwa wala kuteswa. Hata hivyo, hukumu yao itakuwa ya njia maalum.
Kwa ajili ya tofauti ilioko kati ya wema na uovu duniani, tofauti lazima zitakuwako kati ya wale wanaotenda wema na wale wanaotenda uovu (Yak. 4:4; 1 Yoh. 2:15-17). Kwa hivyo, kila mkristo anahitajika kuchukua msimamo maalum kuhusu yale yanayompendeza Mungu na yale ambayo ni uovu.
Mwaliko ni hivi sasa, hata huenda ni nyakati za dhiki tayari. Fanya hima, chagua msimamo. Mrudie Mungu, mwamini Kristo. Kwa yule anayetaka kupokea wokovu, Mungu anasema hivi: "Na roho na Bibi – arusi wasema, Njoo! Naye asikiaye na aseme, Njoo! Naye mwenye kiu na aje; na yeye atakaye, na ayatwae maji" (Ufu. 22:17).
Usipoteze wakati. Fanya hima. Piga magoti na ukatubu dhambi zako katika jina la Kristo. Naye anatuhakikishia kwamba kamwe hatatuacha (Yoh. 6:37). Yeye anangoja kwa hamu ndipo sasa twasoma hivi katika Agano la kale kitabu cha Isaya 1:18:
Mungu anamsamaha usio na kifani (Isa. 55:7). Hata kama umerudi nyuma mara kadha na kuuacha Ukristo, unaweza kuwa na uhakika kwamba utakapomrudia Mungu, yeye hatakukataa. Usiache muovu akudanganye kwamba dhambi zako ni nyingi mno, na hauwezi kupata msamaha. Tubu kila dhambi, na uamini jinsi tunavyoagizwa katika 1Yoh. 1:9 kwamba waweza kupata wokovu.
Waeleze wenzako na kushuhudia kuhusu wokovu wako, na jinsi ambavyo Mungu amekusaidia hata kama kufanya hivyo kwaweza kukakuletea shida. Hayo ni maagizo katika Warumi 10:9-10. Usione aibu kushuhudia kuhusu mwokozi wako, na usinyamaze na kusita kutaja yale mazuri amekutendea. Soma Petro 1, na furahi hata pale unapokumbana na shida na majaribu ya aina aina kwa ajili ya imani yako. Taabu za dunia haziwezi kulinganishwa na maisha ya milele ya baadaye. Twaambiwa hivyo katika 2 Wakorintho 4: 16 - 2 Wakorintho 5:1 Muda ni mfupi sana, na lile unalofanya wakati huu laweza likakufanya upate au ukose ufalme wa mbinguni.
Pale kumalizia Ufunuo, twaelezwa wazi kwamba roho mtakatifu anapoingia ndani yetu pale tunapopokea wokovu, tutakuwa na hamu ya kungoja kurudi kwake mwokozi wetu Yesu Kristo mara ya pili (Ufu. 22:17, 20).