Katika kifungu cha kwanza cha Ufunuo wa Yohana, jambo moja ambalo lajitokeza wazi kabisa ni kwamba maandishi yaliyomo sio maneno ya mzaha ila ni maneno ambayo yatakuja kutokea. Jambo hili lajitokeza katika msitari wa kwanza wa kifungu cha utangulizi katika Ufunuo huu wa Yohana. Pia imeandikwa wazi ni wapi unabii ulio kwenye Ufunuo umetoka.
Twasoma hivi: "Ufunuo wa Yesu Kristo, aliopewa na Mungu awaonyeshe watumwa wake mambo ambayo kwamba hayana budi kuwako upesi; naye akatuma kwa mkono wa malaika akamwonyesha mtumwa wake Yohana" (Ufu. 1:1).
Yohana alitumia njia ya maandishi, na kupitia njia hii akahakikisha kwamba ujumbe huu maalum unawafikia wakristo wote duniani. Katika msitari wa pili, kifungu cha kwanza, Yohana anasema kwamba yale yote aliyoyaandika alifanya hivyo kwa uangalifu sana kwa maana ni maneno ambayo yametoka kwa Mungu, na pia ushuhuda wake Kristo. Yohana anasisitiza kwamba yeye ni mjumbe, na akiwa mjumbe kazi yake ni kuwapa wakristo ujumbe huu kutoka kwa Mungu ambao umewafikia kupitia kwa Kristo. Katika Ufunuo basi, mwandishi Yohana ni mjumbe.
Tukiendelea hadi msitari wa tatu kifungu hiki cha kwanza, kuna agizo hapa kwamba wale watakaosikiliza na kuyashika vyema maneno ya unabii huu watapokea baraka. Twasoma: "Heri asomaye na wao wayasikiao maneno ya unabii huu, na kuyashika yaliyoandikwa humo; kwa maana wakati U karibu" (Ufu. 1:3).
Mtume Petro pia ametilia mkazo sana umuhimu wa maneno ya unabii. Twasoma hivi katika waraka wa Petro kwa watu wote:
"Nasi tuna lile neno la unabii lililo imara zaidi, ambalo mkiliangalia kama taa ing'aayo mahali penye giza mwafanya vyema, mpaka kutakapopambazuka na nyota ya asubuhi kuzuka mioyoni mwenu. Mkijua neno hili kwanza, ya kwamba hakuna unabii katika maandiko upatao kutafsiriwa kama apendavyo mtu fulani tu. Maana unabii haukuletwa popote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu wakiongozwa na Roho mtakatifu" ( 2 Pet. 1:19-21).
Mwangaza wa maneno ya unabii umekuwa ukiangaza kote duniani wakati wote na kuwaongoza walio safarini hapa duniani ambapo kuna giza kuu la kiroho. Mmoja wa wale waliokuwa na imani kubwa sana ni Ibrahimu wa Agano la kale. Yeye aliishi katika hema ugenini, katika sehemu ambazo hakuzielewa vyema wala kufurahia.
Lakini kwa vile yeye alikuwa amepokea maono kuhusu mji ambao tayari umejengwa na Mungu, mji ambao ungekuwa boma lake ( Ebr. 11:10), Ibrahimu aliishi kila siku akiwa na imani kwamba ingawa yeye alikuwa ugenini, tayari alikuwa na makao mbinguni katika mji mpya, Yerusalemu.
Ujumbe katika ufunuo ni ujumbe kutoka kwa Mungu ambaye asili yake ni ile ya utatu – yaani Mungu Baba, Mungu Mwana, na Mungu Roho Mtakatifu. Ujumbe huu katika Ufunuo unajumuisha pia barua zilizoandikiwa makanisa saba katika Asia yaani Efeso. Smirna, Pergamo, Thiatira, Sardi, Filadelfia na Laodikea.
Jambo moja ambalo lazima tulitilie maanani ni kwamba barua zilitumwa kwa makanisa saba.
Nambari hii saba huwa ina maana maalum katika maandishi matakatifu, na hasa katika kitabu hiki cha Ufunuo. Saba ni nambari ambayo ni sawa na kipimo kilicho kamili. Hii ni nambari ambayo haiachi chochote inje – yaani si nusu wala theluthi tu, ila ni kitu kilicho jumla na pia kikamilifu. Kwa hivyo, kwa vile barua zilitumwa kwa makanisa saba, tunaweza hapa kusema bila kusita kwamba makanisa saba haya yanajumlisha kanisa lote la Kristo katika dunia enzi zote.
Wema wa Kristo, akiwa kiongozi wa kanisa kote duniani umefafanuliwa kwa ufasaha sana katika kitabu hiki cha Ufunuo. Ni yeye alitupenda pale tukiwa bado tumo katika dhambi, na akaosha dhambi zetu zote na damu yake. Yeye ni alfa na Omega; yaani wa kwanza na wa mwisho. 'Alfa' ina maana kwamba ni yeye kiumbe nambari moja cha Mungu, na pia yeye ndiye mwanzo wa mpango wa Mungu kuwapa sisi wanadamu wokovu. Nayo 'Omega' ndio mwisho wa kazi ya kanisa la Kristo ambaye kwa ajili yake na kupitia kwake wakristo wamepata njia ya kuingia uzima wa milele.
Katika Ufunuo, Yohana anakutana na kumuona Kristo na kuzungumzia juu yake hivi sasa akiwa yuko anayaona yote yanayotendekea duniani. Yohana anamtaja Kristo kuwa anatembea kati ya visingi vya taa ambavyo vimejengwa kwa kutumia dhahabu, na anapotembea kati ya visingi vyenyewe anaangalia kwa makini yote yanayoendelea. Taa hizi pamoja na visingi vyenyewe twaweza kuvichukua kuwa sawa na vikundi vya wakristo waliokusanyika pamoja. Vikundi hivi ni sawa na vyombo ambamo patawekwa mafuta ya roho mtakatifu. Wakati Wakristo watakapomwagiwa mafuta haya ya roho mtakatifu, basi watang'aa kote duniani kama taa imulikayo katika giza kuu lililoko duniani.
Katika ufunuo, Kristo ameonyesha ama anaonekana na utukufu. Vazi ambalo ni kama joho ambalo amevaa ni refu na linafika miguuni. Ana mkanda au mshipi uliotengenezwa na dhahabu.
Na hii inatilia mkazo utukufu wake. Mavazi haya yanazidisha utukufu wake na kumfanya aonekane kuwa kuhani aliyetoka nyumba ya ufalme.
Nywele zake ni nyeupe, kwa ajili ya hekima aliyonayo. Macho yake ni kama moto na maana yake ni kwamba ana uwezo wa kutoa hukumu ya haki, na pia kwamba yeye hawezi kufa (Omniscient). Pia hakuna kile ambacho chaweza kujificha na kuwa mbali naye.
Miguu yake iliyo kama chuma (brass) iliyochomwa na moto katika sehemu ya kusafisha chuma. Hii nayo ina maana kwamba yeye ana utukufu na hana dosari lolote la uchafu. kwa ajili ya dhambi zetu, amelazimika kupitia kwenye moto kama ule wa kusafisha chuma.
Moto kama huu umeandaliwa na Mungu kuwahukumu wakosaji. Yeye alipitia kwenye moto huo katika Gethsemane, pale msalabani, na hata kaburini. Wakati wa kukumbana na haya yote, yeye hakulalamika wala kusita sita. Ni jambo la muhimu kuwaza hapa kidogo kuhusu haya yote aliyoyavumilia. Kristo aliacha utukufu wa mbinguni kuja hapa duniani akadhihakiwa, akapigwa na kufa akiwa amewekwa kwenye kundi moja na wezi. Hapa ndipo alipouawa, sawa na wezi wenye dhambi.
Katika kitabu cha Isaya twasoma: "Alidharauliwa na kukataliwa na watu; mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Alidharauliwa na wala hamkumhesabu kuwa kitu. Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; lakini tulimdharau tulimdhania ya kuwa amepigwa na Mungu, kuteswa na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, na kwa kupigwa kwake sisi tumepona" (Isa. 53:3-5).
Naye Mtume Paulo pia katika waraka kwa wafilipi anataja mengi kuhusu kifo cha kuhuzunisha cha Mwokozi wetu Yesu kristo. Kifo ambacho kilitokana na dhambi zetu sisi wanadamu. Yeye mtume Paulo anapiga hatua moja mbele na kugusia utukufu usio na kifani uliomjia Kristo kutoka mbinguni. Twasoma:
"Yesu Kristo... ambaye mwanzo alikuwa yu namna ya Mungu, naye hakuona kuwa sawa na Mungu kule kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akwa mtii hata mauti, naam, mauti ya msaaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkarimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba" (Flp. 2: 6-11).
Katika Ufunuo, Yohana anazungumzia juu ya Kristo ambaye akiwa na utukufu yuko katikati ya visingi. Ni Kristo yule yule ambaye twasoma habari zake katika kitabu cha nabii Isaya kwamba wakati wa kujaribiwa, na hata kupelekwa mbele ya wale waliomfanyia mashataka, na kumdhihaki, yeye hakutamka lolote. Alionewa lakini akanyenyekea wala hakufunua kinywa chake (Isa. 53:7).
Ni huyu Kristo ambaye hapa katika Ufunuo ana sauti kubwa inayosikika kila pembeni sawa na mngurumo wa maji baharini. Hakuna awezaye kufanya ubishi, wala kupinga mamlaka, aliyo nayo wakati huu. Matamshi yake sasa ni sawa na kisu chenye makali pande mbili.
Matamshi yake, kama kisu yanatoka kinywani na uhodari ambao unasababisha mgawanyiko, na kufanya haki katika kuhukumu wenye dhambi. Uso wake unang'aa sawa na jua ambalo hutoa giza kote duniani. Mashahidi wake ni kama nyota zilizo kwenye mkono wake wa kulia. Mashahidi hawa ni wao wataleta mwangaza katika dunia iliyochakaa na giza kuu. Miguu yake imetengenezwa na aina ya chuma maalum (brass), ambayo ina nguvu baada ya kutengenezwa kwa ustadi. Kwa hivyo, ni sharti wafuasi wake nao wajitolee kufanya yale yaliyo ya utukufu.
Wanapofanya hivyo, wafuasi hawa ni lazima wawe tayari kukumbana na matatizo ya aina aina. Matatizo haya ni sawa na mtambo ambao kazi yake ni kuwandaa na kuwafanya wawe wakristo bora zaidi jinsi vile chuma huchomwa na moto ili iwe stadi na bora zaidi.
Ufunuo wa Yohana ni kitabu ambacho kinatilia maanani kwa kiwango kikubwa sana mengi yanayohusu Kristo. Kwanzia pale alipozaliwa, wengi walimpokea kwa njia mbali mbali. Mara tuu pale alipozaliwa, Simeoni akitaja kumhusu alisema: "Tazama huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa" (Lk. 2:34).
Kwa muda wa miaka miaka 2000 hivi, Kristo amekuwa chanzo cha maisha mapya kwao mamilioni ya watu. Wengi nao wamepotea na kuangamia kwa sababu wamemuacha na kufuata njia zao wenyewe, njia zielekeazo kwenya giza.
Kwa kifupi basi, kitabu cha Ufunuo kinaeleza na kutilia mkazo kwamba Kristo ni Mwokozi, pia ni yeye anayehukumu. Kwanza kabisa, Kristo anaonekana kuwa Mwokozi na pia kongozi wa waKristo, kwa ajili ya kuwa kichwa cha kanisa duniani. Akiwa kiongozi, anatembea, na pia yuko katika vikundi vya Wakristo, akiwatia moyo wakati wa shida, hasa wale walio wakristo wa kweli. Pia anawakosoa wale ambao wanaenda kinyume cha maagizo.
Na mwisho, anaendelea kutoa wito kwa wale ambao hawana imani kamili na hawajakubali wokovu ila wao wanashiriki katika madhehebu, nayo imani hii yao ni ya juu tuu. Anawataka watubu dhambi zao ili wapokee wokovu wa kweli.
Utukufu ulio katika kanisa, na Kristo akiwa kama mfalme haya yote yanahusiana moja kwa moja na kazi yake maalum ya kuleta wokovu kwetu sisi wanadamu.
Pili: Katika Ufunuo, Kristo amejitokeza kuwa jaji mkuu ambaye atawahukumu wale wote ambao hawakubali kwamba yeye ni Bwana. Twaona pia kwamba, hadi dakika ya mwisho, akiwa jaji, Kristo anawapa wale wasio na imani fursa ya kukubali kuwa yeye ni mwokozi.
Na mwisho: Katika Ufunuo, jambo moja ambalo latiliwa mkazo sana ni kwamba wakati wa mwisho, baada ya yote haya kutokea, wakati ambapo wote ambao ni wafuasi wa mpinga Kristo mkuu watahukumiwa, nabii mkuu wa uongo atahukumiwa. Hukumu yenyewe itakuwa kupitia kisu chenye makali ambacho kimo kinywani mwa mwokozi wetu.
Katika mambo haya yote; yaani wema, utukufu na hukumu, lile ambalo ni la muhimu sana lahusu uhusiano aliye nao kila mmoja wetu na kristo. Swali kuu hapa ni hili:" Je, wewe ni mfuasi wa Kristo au la?" Hili swali ni chanzo ai msingi wa yale ambayo Yohana mtakatifu anasema katika Ufunuo: Msujudie Mungu. Kwa maana ushuhuda wa Yesu ndio roho ya unabii (Ufu. 19:10).
Kristo anaokoa. Pia ni yeye atakayehukumu Wakati ule wa mwisho saa ya dhiki itakapofika, dunia ambayo haikatubu, wala kumkubali Kristo itakuja mbele ya kiti cha enzi cha hukumu, na hapa kuwa nafasi yao ya mwisho kutubu na kumkubali Kristo kama mwokozi.
Katika kitabu hiki cha Ufunuo, yale tunayosoma ni yale Kristo anasema moja kwa moja na kumueleza mtume Yohana. Yohana naye, wakati huu amejawa na hofu kuu na ni mnyeyenyekevu mbele ya Bwana. Kwa kweli wakati huu, Yohana anaanguka kama maiti miguuni mwa Bwana. Na kabla ya kumueleza lile la muhimu kabisa kuhusu hukumu ya mwisho, na kuhusu uharibifu utakaotokea, Bwana ananyoosha na kuuweka kwenye sehemu ya bega la Yohana huku akisema: “Usiogope.” Yeye bwana wetu ameshinda nguvu za muovu tayari, pale alipopita mauti, kwa hivyo, yule aliye na imani, ana ni wake mfuasi halisi ataepuka hukumu. Haya twayapata katika kitabu cha Yohana Mtakatifu: "Amin, amin nawaambia, yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yu na uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani” (Yn. 5:24).
Mpangilio wa Kitabu cha Ufunuo.
Tukirudi kifungu cha kwanza cha Ufunuo, msitari wa kumi na tisa, (Ufu.1:19) Yohana amepewa agizo kwamba ayaandike haya ambayo ameyaona, na yale yaliyopo, na yale yatakayokuja. Kristo hapa anatumia utaratibu maalum katika kutoa agizo lake kwa mtumishi wake Yohana. Ni bora kuelewa vyema utaratibu unaofuatwa na mwokozi wetu; na hii itakusaidia kuelewa vyema yote yaliyo kwenye ufunuo huu. Yako matukio aina tatu ambayo yametajwa:
· Kwanza kabisa, Yohana anaagizwa ayaandike yale ambayo ameyaoana. Yaani, hapa anaagizwa aandika hasa kuhusu Kristo amaye amemuona akiwa katika utukufu wake wote wa mbinguni kati ya misingi saba ya taa.
· Pili, Yohana anaagizwa aripoti kuhusu yale yaliyopo. wakati alipopokea maono haya ya Ufunuo akiwa katika kisiwa cha Patmo mwaka wa 95 AD (baada ya kifo cha Mwokozi wetu Kristo). Huu ulikuwa wakati ambapo kanisa au Ukristo ulikuwa ukienea kwa haraka sana. Bado Ukristo unaenea sawa na hapo mwaka wa 95 AD, lakini tofauti ilioko hivi sasa ni kwamba sisi tunaishi nyakati za mwisho, naye Yohana aliishi nyakati za mwanzo.
· Na mwisho, ufunuo wahusu yale ambayo yatatokea baada ya mwisho wa dunia.
Kwa hivyo ni wazi kwamba kitabu cha Ufunuo kimeandikwa kwa kufuata utaratibu wa miaka.
· Katika kifungu cha kwanaza twasoma habari kuhusu utukufu wa Kristo kote duniani.
· Kifungu cha 2 na 3 vyahusu kuenea kanisa la Kristo kote duniani.
· Katika kifungu cha 4 na 5, tuna maono hapa yanayohusu utukufu wa kanisa la Kristo.
· Kifungu cha 6 hadi 19:10, kuna habari kuhusu miaka ile saba ya dhiki kuu.
· Katika kifungu 19:11 - 21, tuna maelezo yanayohusu kurudi kwake mwokozi wetu Yesu kristo.
· Katika kifungu cha 20: 1- 6, twapata maelezo kuhusu miaka 1000 ambayo ni enzi ya amani.
· Na katika kifungu cha 20: 7-15, twasoma mengi kuhusu hukumu ya mwisho.
· Tunakamilisha kitabu cha ufunuo katika kifungu 21 na 22 kwa kupokea habari kuhusu mbingu mpya na dunia mpya baada ya hukumu.
Ingawa matukio haya yote ya unabii yamefuata utaratibu maalum wa miaka – mwanzo hadi mwisho; matukio yanayohusu dhiki kuu (kifungu 6 - 19) yameandikwa kwa kufuata utaratibu unaohusu matukio yenyewe jinsi yatakavyofuatana, na sio kwa kufuata miaka ya matukio yenyewe. Matukio katika kifungu cha 6 yote yanatokea katika muda wa miaka saba. (Na hii ni sawa na wiki moja ambayo huwa na siku saba).
Yule farasi mweupe ambaye ni mpinga Kristo anayejitokeza kuwa kama mwana mrithi mleta amani anajitokeza katika wakati ule wa mwanzo wa dhiki. Farasi wa rangi nyekundu ni wa vita, naye mweusi ni wa njaa, na wa rangi ya kijivu ni wa kuleta kifo – hawa farasi wote wanajitokeza baada ya kati ya wiki (yaani baada ya nusu ya saba).
Wale waliokufa kwa ajili ya imani yao wakati wa muhuri wa tano wanakusanywa pamoja wakati wa dhiki. Nayo yale mabadiliko ya kutisha na ya ajabu angani yanayohusu nyota na kadhalika, haya ambayo yametajwa yatatokea wakati wa muhuri wa sita, haya yote yatatokea pale mwisho wa nyakati hizi za dhiki kuu.
Wale wayahudi ambao wanatajwa katika ufunuo kifungu cha 7:1-8, wataokolewa pale mwanzo wa wa dhiki kuu. Wakristo ambao wamekufa kwa ajili ya imani yao ambao wametajwa katika Ufunuo 7:9-17 watakusanywa pamoja baada ya siku tatu au baada ya nusu ya muda huu uliowekwa yaanii muda wa juma moja.
Katika Ufunuo 12 na 13; matukio yote ambayo yameandikwa yahusu matukio katikati ya muda ule wa dhiki kuu. Na katika Ufunuo 17, kuna Babeli ya uchawi (mystical Babylon) na maajabu ambayo inajitokeza hapa pale mwanzo wa juma hili. Anatupiliwa mbali na kuawa baada ya miaka tatu na nusu. Babeli ambao ni mji wa biashara unatajwa katika ufunuo 18. Hii itatokea pale mwisho wa dhiki kuu.
Kanisa la bandia ambalo litajitokeza katika Ufunuo 17, na hili ni kanisa la kimataifa. Hili litajitokeza katika nusu ya kwanza ya muda wa dhiki kuu. Kanisa hili litaachwa na kutupiliwa mbali baada ya miaka tatu na nusu ya dhiki kuu. Mji ule mkuu wa Babeli ambao unatajwa katika Ufunuo 18 utaharibiwa na kubomolewa kabisa katika miaka ile ya mwisho ya dhiki kuu.
Wanaoamini kwamba Hesabu ya Unabii ya Miaka elfu moja , hakika ni miaka hiyo (Millennialists) Kuna wale ambao huelewa na kuyachukua yale yalioko katika maandishi matakatifu ya Biblia kulingana na jinsi maandishi yenyewe yalivyo. Kwa mfano hesabu ya miaka elfu moja ambayo inatumiwa katika maneno ya unabii, wao wanachukua hesabu hii kuwa ni miaka kamili elfu moja. Hawa huitwa millennialists. Neno hili millennialists limetokana na jina la kiLatin ambalo lina maana "elfu Moja." Kwa hivyo, wale ambao ni millennialists huchukua kwamba kuna miaka elfu ambayo itapita, miaka ya amani itakayofuata kuja kwake Kristo.
Wakati fulani, hawa pia huitwa pre-millennialists, na jina hili hapa linatokana na sababu kwamba wanaamini Kristo atarudi kabla ya millennium au kabla ya miaka elfu moja.
Millennialists huchukua maandishi matakatifu kuwa na maana ile iliyo katika maneno yaliyoandikwa. Wakati fulani, maandishi matakatifu huwa na maana iliyo mbali na ile ambayo imeandikwa. Kwa mfano yuko mnyama (dragon) wa vichwa saba anayetajwa katika ufunuo, huyu anachukuliwa kuwa shetani. Hii ni wazi, na hapa hwa pre-millennialists wanachukua mnyama huyu kuwa shetani.
Lakini kwa mfano pale Biblia inapotaja mambo yanayohusu Yerusalemu, Dhiki kuu (tribulation), mpinga Kristo (Antichrist), vita vikuu Har-Magedoni, kutekwa na kufungwa shetani wakati Kristo atakaporudi, hatuwezi tukachukua maandishi haya kuwa na maana tofauti na ile maana ilio katika maneno yenyewe. Millennialists huelewa maandishi matakatifu kwa njia hii. Ushauri wetu hapa ni kwamba ikiwa lile lililoandikwa laeleweka vyema, hakuna haja kutafuta maana iliyotofauti na ile inayoeleweka.
Wako wale ambao nao wanaamini kwamba maandishi matakatifu yana maana iliyojificha ambayo haiwezi kueleweka moja kwa moja. Kati ya hawa wako wale ambao hawachukui maandishi matakatifu kwa njia ile yalivyoandikwa kwamba kutakuwa na miaka elfu moja moja ya imani baada ya kuja kwake Kristo mara ya pili.
Wanaoamini kwamba tuko katika muda ule wa Miaka elfu moja (Amillennialists). Wako waKristo ambao huchukua yale yaliyo katika maandishi matakatifu, na kuyaangalia kwa undani sana hadi kiwango ambapo wao hukosa kuelewa yaliyomo vyema. Kati ya hawa, wako wale ambao hawaamini kwamba kuna ile enzi ya amani itakayofuata kuja kwake Kristo, na kwamba amani inayotajwa hapa ni amani ambayo yaweza kuoenekana wazi. Wenye imani hii husema kwamba amani inayotajwa ni amani ya kiroho ambayo haiwezi kuonekana na macho. Wao husisitiza kwamba muda huu wa amani uko nasi, na hatujui uko nasi kwa vile amani yenyewe ni ya kiroho. Kwa hivyo muda wenyewe sio miaka 1000, na shetani hajafungwa kabisa ila amefungwa na mnyororo mrefu na anaweza kutembea hapa na pale na kutenda uovu wa aina aina kote duniani.
Wanaoamini Kwamba Wakati wa Karne Kuu uko mbele yetu (Post-millennialists). Na wako wale ambao nao wanaamini kwamba kanisa lina uwezo wa kubadili dunia na kuleta hali ile ya utawala wa amani uitwao millennium. Wao wansema kwamba Kristo atarudi tuu baada ya muda huu, ambao ni wakati wa millennium. Hawa nao huitwa post-millennialists.
Amillennialists hawaamini katika unabii wa agano la Kale kuhusu taifa la Israeli. Wao hawaamini taifa hili litafufuka kiroho na kuwa taifa kuu jinsi vile maandishi matakatifu yanavyosema. Wao huchukua kanisa kuwa sawa na taifa la Israeli. Amillennialists pia hupuuza tukio lile ambalo limeandikwa kwamba kuna wakati tukiwa wakristo tutanyakuliwa na kukutana na Kristo katika mawingu. Kwa kifupi, wao huchukua unabii ulioko katika Ufunuo kuwa ni mambo ambayo hayawezi kutiliwa maanani kwa ajili matukio yaliyomo tayari yametokea.
Wao hupuuza utaratibu ulioko katika Ufunuo, utaratibu ambao umepangwa kufuatana na miaka kuhusu jinsi vile matukio fulani yatatokea siku za mwisho. Wanachukua kwamba ile miaka 1000 ambayo imetajwa katika Ufunuo 20 ni muda ambao tayari tunauishi, na haifai tuendelee kusubiri tukingoja muda huo.
Kwa kweli maoni kama haya ni hatari kwa maana yanawafanya wengi wapuuze unabii. Matokeo huwa, wengi hawatilii maanani umuhimu wa kujiweka tayari kiroho kwa ajili ya kuja kwake Kristo mara ya pili. Hatari kuu ilioko ni kwamba wakristo wengi, kwa ajili ya imani hii, hukosa kujiweka tayari na hivyo kujiingiza katika mengi ya kidunia. Na hapa wengi hujikuta wanajishughulisha zaidi na mambo yanayohusu uhusiano kati yao, siasa, na mambo fulani yanayohusu jamii.
Uhusiano wao na Mungu huwa hawautilii mkazo. Wengi hata husahau kwamba maandishi matakatifu yatuonya tuwe tayari, na kwamba Kristo atarudi tena. Wao hupuuza umuhimu wa kujiweka tayari kwa ajili ya kuja kwake Kristo mara ya pili.
Na sasa tuangalie kikundi kiitwacho millenialists. Walio katika Kikundi hiki nao wanatilia mkazo ukweli wa kimsingi wa yale yaliyo katika maandishi matakatifu. Wakristo katika kikundi hiki huweza kuyaona matukio duniani kwa njia inayokubaliana kwa karibu sana na unabii.
Wakristo ambao ni millennialists huwa wanaweza kuyafafanua matukio duniani hivi sasa wakitumia maneno ya unabii, na kwa hivyo wanaweza kuona utaratibu wa kiBiblia katika mambo yote yanayoendelea hivi sasa duniani.
Wao wanaweza kuepuka mtego ule unaowakumba wale amillennialists wa kukosa kuwa tayari kwa ajili ya imani kwamba tayari shetani amefungwa, na tunaweza kukaa kimya na kusubiri tuu na kufurahia yale yaliyomo duniani wakati huu. Badala yake wanajiona kuwa kama wageni katika dunia ya uovu (1 Yn 5:19). Katika mawazo ya aina hii basi, kuna vita ambavyo vinatarajiwa kati ya giza na mwanga.
Premillennialists nao wanajua tukokatika saa aya hatari na kwamba kanisa linaelekea mwisho wake hapa duniani. Kwa hivyo wao wanatumia muda wao kuwaonya wenzao kuhusu umuhimu wa kujiandaa kukutana na Kristo.
Mkazo unatiliwa kazi ya uinjilisti; kazi ambayo ni ya kutii agizo kuu katika maandishi matakatifu, kazi ya kueneza injili kwa mataifa yote. Na zaidi, maneno ya unabii yanawataka watu wote wafuate utaratibu wa kiBiblia katika maisha yao, hasa katika mambo ya kiroho, ikiwa ni njia moja ya kujitayarisha kwa ajili ya kurudi Kristo. Wao pia wanangoja kwa hamu kurudi kwa mwana harusi (bridegroom), ambaye atawapeleka makao maalum ambayo ameyandaa.
Ikiwa wewe ni mmoja wa wale walio katika kikundi hiki cha millennialists, basi usife moyo wala kutupilia mbali yaaleyaliyo katika kitabu hiki. Sisi hatuhusiki na maneno ya masomo ya dini (Theology), ila yale tunayonuia kuyazingatia katika kitabu ni yale ambayo ni ukweli ulio katika kitabu hiki cha Ufunuo. Jinsi vile jina lilivyo, Ufunuo ni kitabu ambacho kinatufunulia yale yaliyo mbele yetu au yale yatakayokuja ili tuyajue mapema na tuwe tayari.
Kuna ishara au alama ambazo ni za kutisha na ni vigumu kuzielewa katika Ufunuo, na sababu moja ni kwamba aliyeandika Ufunuo, Mtume Yohana alitumia lugha ya zamani, na matukio anayozungumzia yanaweza kutafautiana sana na vile dunia ilivyo hivi sasa, na pia huenda ikawa ilikuwa ni vigumu kwake Yohana kuzungumzia mambo yanayohusu zana za kivita na technologia ya kisasa kwa njia ya kawaida, na hata vita vile vya nuclear na kadhalika.
Nakualika tuwe pamoja katika safari hii yauvumbuzi katika ghala hili kuu la mambo yatakayotokea nyakati za mwisho. Tutagundua utajiri wa mapenzi na uwezo wa Kristo kutuokoa. Pia tutapokea maonyo kuhusu hukumu kali inayowangoja wale ambao hawajamjua Mungu, na mwanawe Yesu Kristo ili wapokee wokovu.