Saa Ya Giza Kuu Yaja

Kimeandikwa na Prof. Johan Malan Na Kutafsiriwa na David Ang'ang'o

Abstract: The Coming Hour of Darkness, by Prof. Johan S. Malan of the University of Limpopo, Polokwane, South Africa. Swahili translation in 1999 by David Ang'ang'o of Trans World Radio in Nairobi, Kenya. This is an exposition of the book Revelation.

 

 

Yaliyomo

Utangulizi

1. Utukufu wa Kristo

2. Kuenea Kanisa

3. Kunyakuliwa!

4. Mpinga Kristo

5. Babeli Yafufuka

6. Taifa la Israel Katika Dhiki Kuu

7. Vita, Magonjwa na Mikasa Mbali Mbali

8. Ufalme wa Masihi na Viumbe Vipya

9. Imekwisha!

10. Mbinu ya Biblia ya Kujiokoa

 

Utangulizi

Ufunuo ni kitabu chenye maonyo kwa watu wote. Hatari na hukumu kali inawangoja wale ambao wanapuuza maonyo haya ya unabii. Maonyo yaliyomo kwenye Ufunuo yameelekezwa kwa wafuatao:

1.   Kanisa la Kristo linaonywa kuhusu hatari zilizoko katika dunia hii ya maovu tunapokaribia dhiki kuu. Wenye imani wanaonywa wajihadhari na uongo na waendelee kuimarisha na kushikilia imani yao wakati wa majaribu haya: Na yeye ashindaye na kuyatunza matendo yangu haya hata mwisho, nitampa mamlaka juu ya mataifa (Ufu. 2:26).

2.   Wakristo ambao wameacha njia na kurudi kinyume cha wokovu wao, pamoja na makanisa ambayo yanajihusisha katika uovu kama upokeaji hongo, ulaji rushwa, na uzinzi (Ufu.2:22), hawa wanaonywa kwamba wataingizwa katika muungano wa dini za uongo ambazo zimemkubali mpinga Kristo (Ufu.17:5), na baadaye kumalizwa na huyo mwovu (Ufu.17:16).

3.   Mataifa yanaonywa kwamba malkia wa amani ya uongo atawaunganisha katika jumuiya mpya ya Babeli ambapo watatupilia mbali mbali haki zao (Ufu. 13:3). Watanyanyaswa kisiasa na serikali za dunia (Ufu.13:7), na kulazimishwa kuisujudu sanamu chini ya uongozi wa nabii wa uongo (Ufu. 13:15), na pia kuteswa katika utaratibu wa kiuchumi mpya utakaoanzishwa na huyu muovu ambapo mtu awaye yeyote hawezi kununua wala kuuza, isipokuwa ana chapa ile ya muovu, kwa kifupi utaratibu ambapo hakuna matumizi ya pesa (Ufu. 13:16-18). Pia watadhuriwa na vita vikubwa na maafa ya ajabu na pia  maradhi na magonjwa mbali mbali.

4.   Taifa la Israeli mara nyingi limeonywa kuhusu masihi wa uongo siku za mwisho (Dan. 9:27, 11:31; Mt. 24:15; Yn. 5:43). Yeye anaitwa mnyama katika Ufunuo 13:1. Mbali  na kikundi cha wachache ambao wameweka imani yao katika masihi wa kweli, taifa hili litafikia makubaliano na na huyu masihi wa uongo, na baadaye kusukumwa karibu kuangamizwa kabisa watakapogundua uongo baada ya miaka mitatu na nusu ya utawala wake. Baada ya hapo watavunja makubaliano hayo na kuachana naye (Mt. 24:15-22; Ufu. 12:13-16).

5.   Wafuasi wa masihi wa kweli wanaonywa kuhusu wakati wa dhiki. Wanaonywa juu ya umuhimu wa kuwa tayari kiroho ili waweze kuepuka saa ile ya giza kuu (Lk. 21:36). Watakuwa mbinguni wakati muhuri wa kwanza wa hukumu katika Ufunuo utafunguliwa (Ufu. 4:4; 5:9). Sawa na wale waliokuwa na imani wakati wa Nuhu na Lutu, wenye imani kamili wakati huu watakaokolewa kutoka kwa maafa kabla hasira ya Mungu haijafikia dunia yote yenye dhambi.

6.   Wale ambao hawatakuwa tayari wakati wale wenye imani watakaponyakuliwa, pamoja na kikundi cha wale ambao watapokea wokovu wakati wa utawala wa taabu wa mpinga Kristo (Ufu. 7:9-17), wanaonywa kwamba watalipa gharama kubwa kwa ajili ya kuwa watu waliokosa imani na kuwa na uovu (Ufu. 6:9-11). Na hata ingawa  wanataabika  hata kwa ajili ya imani yao, hawa hatimaye watashinda nguvu za giza (Ufu. 12:11). Kifungu cha mwisho katika Ufunuo kina maneno ya kutia moyo na kuwaongeza nguvu wakristo.

7.   Onyo la unabii kwa watu wote lapatikana katika maneno haya ya mwokozi wetu Yesu Kristo: “Angalieni, mtu asiwadanganye" (Mat. 24:4). Ni ombi langu kwamba kitabu  hiki kitakusaidia kujiandaa kukabiliana na yale yaliyo mbele, na pia kusimama imara katika ngome ya wokovu.

 

Johan  S. Malan

University of Limpopo

Polokwane

South Africa